NANUKUU
Kabla ya mimi na yeye kuwa chini ya Tamadunimuzik iliyoanza mwaka
2011; Nikki mbishi ni msanii ambaye nimeanza kumsikia baada ya miaka ya
2000 kugawanyika. Uwezo wake wa kisanaa sio kitu ambacho napaswa
kubishania, itoshe tu kusema jamaa anajua. Najua anatambua uwezo wangu
katika uandishi na ndiye aliyethubutu kunipachika jina la "Nyambari
Nyangwine" japo sikuwahi kulipenda lakini watanzania wakiamua wameamua.
Nidiklee interesti kwamba Mimi na Nikki tunafahamiana na tumewahi na
tunafanya kazi pamoja kama Tamadunimuzik japo kuna baadhi ya mambo ya
muziki nimeyaweka kando lakini ntaendelea kuwa sehemu ya Tamadunimuzik
kwa kadri nitakavyobarikiwa. Kwa hivyo makala hii haitaegemea upande
wowote kama ambavyo nilifanya makala iliyomhusu Bonta japo baadhi yenu
mliishutumu Tamadunimuzik lakini makala hii na zijazo zibakie
kuheshimiwa kama mawazo yangu peke yangu na sio ya kikundi chochote.
Mwaka jana mwezi kama huu niliwahi kuweka "Post" katika mtandao wa
jamii nikisema kuwa wakati mwaka 2014 ukiwa unaelekea kufikia tamati
wasanii Nikki Mbishi na One the incredible walipewa ushauri na ndugu
Fredrick Bundala maarufu kama Sky Walker ambaye ni mhariri wa Bongo 5
kuwa wakitaka kufanikiwa hawana budi kufanya kile ambacho kundi la Weusi
wamefanya mpaka wamefikia hapo walipo. Ama kwa Lugha nyingine Nikki
Mbishi afuate nyayo za weusi ili afanikiwe.
Katika makala hii
nitamzungumzia zaidi Nikki Mbishi japo makala ile ya ndugu
Fredrick Bundala (Sky Walker) ambaye katika makala hii nitatumia
jina “Mwandishi” kumwakilisha ilikuwa imeandikwa kuwalenga watu
wawili yaani Nikki Mbishi na One the Incredible. Nitafanya
hivyo kwa sababu haya nitakayoyajadili yanamhusu zaidi Nikki
Kuliko One the Incredible. Kwa ambao hamkuwahi kuisoma makala
hiyo inapatikana katika tovuti ya Bongo5 ikiwa na kichwa cha
habari “Kwanini Nikki Mbishi na One The Incredible wanapaswa
kujifunza kutoka kwa Weusi”.
Kumwambia Nikki Mbishi afuate
njia ambazo weusi wamepitia ili afanikiwe kimuziki ilikuwa
kumkejeli. Sababu kubwa ni kwamba wakati ushauri unatoka ndio
wakati ambao Nikki Mbishi alikuwa na Mgogoro mkubwa na Weusi
hivyo ingewezekanaje umwambie awe kama watu ambao ana mgogoro
nao. Naamini ndio ulikuwa wakati muafaka ambao Nikki mbishi
alikuwa akiamini amemaliza changamoto anaweza “ku –create enemity”
na isimuathiri kisanaa tofauti na alivyoamini katika kibao
chake cha “Punchline”.
Mwandishi anaweza pia kuwa sahihi
kwa sababu Nikki alishawahi kusema kwamba yeye hajakamilika
“sometime anakosea, msije mkahamasika mkamuiga na kupotea”. Hilo
linawezekana kabisa ndani ya kizazi hiki ambacho “kinakua
kinaona na kusikia, kudadisi, kujaribu na mwisho kutumbukia”.
Yote kwa yote Nikki mbishi ni Mc ambaye anaamini katika nyayo
zake sio nyayo za mtu mwingine ili kupata mafanikio. Alishawahi
kusema “andagraundi wanawishi kwa kila hali na mali, wakifata
nyayo (zake) hakika watafika mbali”. Sasa kama wanaofata nyayo
zake wanaweza kufika mbali vipi mwenye nyayo ashindwe kufika
mbali.
Mwandishi alishawahi pia kueleza chanzo cha Mgogoro
wa Nikki na Memba wa weusi kimojawapo ni Jina “Nikki” ndio
kukawepo Tension kati ya Nikki Mbishi na Nikki wa Pili
(Bundala, 2012). Sijui ndio kisa Nikki Mbishi kuuliza “Kivipi
Nikki wa pili wa kwanza hajulikani?” na labda ndio
kilichomchochea Raf Mc wa utengwani kusema “(a)nawachana wote
manikki wawili”
Mwandishi anaendelea kueleza kwamba
mstari huo wa kuhoji kivip nikki wa kwanza hajulikani? Ndicho
kilichopelekea Rama D ambaye alikuwa ameshirikishwa na Nikki
Mbishi kuimba kiitikio cha wimbo wa Punchline kuomba sauti zake
ziondolewe katika kibao hicho kwakuwa hakutaka kugombana na Joh
Makini ambaye inasemekana hakuwa akimpenda Nikki Mbishi. Hivyo
ndio baadaye Grace Matata akaimba kiitikio cha wimbo huo
(Bundala, 2012).
Hii inanikumbusha kisa nilichowahi
kukisikia kwamba, mgogoro wa Nikki na Weusi ulichochewa zaidi
na shoo moja ya Dar Live. Katika shoo hiyo Nikki alihudhuria
kama mtazamaji na wasanii wengine waliokuwepo ni baadhi memba wa
weusi na Fid Q. Fid Q alipopanda jukwaani alimuita Nikki
mbishi katika jukwaa kumpa tafu. Kitendo hiko hakikuwapendeza
mmoja kati ya memba wa weusi hali iliyomfanya kutoa maneno
ambayo yalipokuja kumfikia Nikki Mbishi hayakumpendeza.
Mwandishi alionesha yuko “Fair” mwanzoni mwa makala yake kwa
kutambua uwezo wa Nikki Mbishi kwa kusema anamkubali, hana
mpinzani katika Mitindo huru na pia japo yeye amepitia maisha
ya kuandika mistari lakini hawezi kufikia hata robo ya uwezo wa
Nikki (Bundala, 2014). Kama unazikumbuka nyimbo za Sky Walker
alizotoa hasa kipindi anatangaza Radio Free Africa (RFA) unaweza
kukubaliana ama kutokubaliana kauli yake hiyo.
Kabla ya
makala hiyo ya mwandishi, Nikki Mbishi alishawahi kusema kwamba
“(yuko) kwenye Mainstream ya Underground” yaani kwa kiswahili
rahisi ni kwamba “yuko kwenye mkondo mkuu wa Hip Hop ya
handakini (Underground Hip Hop)”. Kwa mujibu wa mwandishi
anasema Underground Hip Hop ni Hip Hop ambayo iko nje ya mfumo
wa biashara kwa sababu hujiusisha na uandishi wa mashairi
Conscious yaliyo chanya na yasiyo ya kibiashara (Bundala, 2014).
Nikki alishasema kwanza “kufunza ndo kazi yangu na mziki
kwangu ni ajira”. Mziki huo wa Underground Hip Hop ndio ambao
Nikki aliamini ndio ajira yake lakini mwandishi alimshauri
kwamba kufanya Underground ni kupoteza muda tu kama anafanya
muziki kupata chochote labda kama anafanya kujifurahisha tu.
Underground Hip Hop haivutii mkondo mkuu wa biashara itaishia
kumpa sifa tu. Kibongobongo mashabiki hawanunui kazi za
Underground tofauti na mbele ambapo wasanii wa aina hiyo ya
muziki wana maisha mazuri kwa sababu mashabiki wananunua kazi
(Ibid).
Mwandishi alitamani Nikki afanikiwe kama Weusi
alitamani kuona siku moja akipost picha katika mitandao ya
kijamii akiwa airport akiwa anawahi shoo za mikoani kama
wanavyoweka weusi hasa hasa Joh Makini. Si unajua mambo ya
ku-post “Mwanza..niko njiani nakuja… tukutane Rock Bottom” huku
picha ikisindikizwa na selfie akiwa kwenye kiti cha ndege huku
mpiga picha akihakikisha dirisha duara linaonekana. Msanii gani
hapendi…??
Nikki alijipambanua daima kama msanii “fanisi
mwenye fikra yabisi” lakini mwandishi alimshauri kukubali
mabadiliko katika Hip Hop asiwe mhafidhina (conservative) hata
kwenye mdundo wa kapuka anaweza kuchana. Nadhani hilo limejibiwa
juzi katika wimbo wake uitwao ‘Indebe’ ambapo katika wimbo huo
anasema “wengine wana-judge jinsi navyobadilika”. Kumbe Nikki
Mbishi anajua kuwa anabadilika? Unaweza kujiuliza ni nini?
Lakini katika ubeti wa pili mwishoni anakujibu kuwa anajua kuwa
“wengine wanakatwa mizuka, eti kisa… amefanya kapuka”. Kwa hivyo
nikki kachana kwenye biti ya kapuka kama Sky Walker
alivyoshauri.
Nikki pia alishauriwa na mwandishi kuchagua
midundo mizuri na kuachana midundo migumu kwa sababu zinasikika
kama za miaka ya 90 ambazo ni za kizamani na zisizo rafiki
masikioni mwa mashabiki ambao hawana uelewa na beat hizo ngumu.
Mwandishi kwa kujua kwamba Duke Tachez na Watayarisha midundo wa
Tamadunimuzik wamejikita katika utayarishaji wa midundo ‘Underground
Hip Hop’ ambayo yeye hataki Nikki aendelee kutumia akashauri
Nikki ni Lazima afanye kazi na watayarishaji wengine nje ya
Tamadunimuzik.
Nikki ameufanyia kazi ushauri huo japo ni
kweli hii sio mara ya kwanza kufanya na maprodyuza wengine ama
katika midundo ambayo sio ya Boom Bap. Kabla ya kuwa Mlab
wenye kumbukumbu nzuri mtakumbuka alishawahi kufanya Ngoma
ziitwazo “Kichaa cha Mbwa” na “Things Fall Apart”. Baada ya
ushauri huo kutoka kwa Sky Walker ni kama Nikki ameamua
kuusikiliza au kaamua kwa maamuzi yake mwenyewe kufanya nyimbo
ambazo haziko katika mahadhi ambayo tumemzoea. Nikki katika
mixtape yake ya hivi karibuni “Ufunuo wa Unju Bin Unuq”
amefanya nyimbo kama Tulia (R&B beat), Unachonipendea (Dance
Hall Beat), Indebe (Kapuka Beat) na Tembo (Afro Beat).
Lakini pia mkumbuke ameshawahi kufanya kolabo katika wimbo wa
‘Joto Hasira’ na hivi karibuni kashirikishwa na Pinda bway
katika kibao kiitwacho ‘Turn Up The Music’ ambazo zote sio
midundo ya Hip Hop. Huyu Nikki wa sasa ni tofauti na yule
ambaye halikuwa anachagua midundo ya kuchania sitaki kusema
ameamua kuufata ushauri wa mwandishi. Pia sitaki kusema kuwa
Nikki mbishi anatakiwa kuufata ushauri ila auzingatie wa Nash Mc
kwamba Beat za Baibuda, kiduku, za kinaijeria vyote asivitake
achague moja tumuelewe.
Ni kweli mwandishi alitaka kumuona
nikki mbishi akibadilika badilika kwenye kuchana katika midundo
tofauti tofauti kama ambavyo Weusi hufanya na ndio maana
makala yake ikawa na kichwa kisemacho Nikki Mbishi anapaswa
kujifunza kutoka kwa weusi. Nahisi mwandishi atakuwa anafarajika
kuona angalau ushauri wake umefanyiwa kazi.
Kuna wachanaji
wengi leo hii wanachana wanaeleweka ambao wanatamani kuwa kama
Nikki Mbishi lakini Nikki mwenyewe anajikataa kama alivyosema
kwenye moja ya mistari yake. Napata shida kuelewa kama Nikki
mbishi anafata Nyayo zake au anafata nyayo za weusi kama
mwandishi alivyoshauri. Najiuliza tu kama anafata nyayo za Weusi,
Je hao wanaofata nyayo zake anawaachaje? Au ndio atatimiza neno
lake kwamba hawezi kutabiri wala kubashiri wapi ataishia.
Imeandikwa na
Malle Hanzi
O715076444
©2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
-
❝BABU MWENYE NYUMBA❞ {♡Love Story♡_____Part..19} ∪₥ri_____+ ℳtunzi: ₲eofrey Mustafa, ₳rtist Jafa ✍ ℳaahali: Dar es salaam🇹🇿 ₩ha...
-
❝BABU MWENYE NYUMBA❞ {♡Love Story♡_____Part..29} ∪₥ri_____+ ℳtunzi: ₲eofrey Mustafa, ₳rtist Jafa ✍ ℳaahali: Dar es salaam🇹🇿 ₩ha...
-
❝BABU MWENYE NYUMBA❞ {♡Love Story♡_____Part..26} ∪₥ri_____+ ℳtunzi: ₲eofrey Mustafa, ₳rtist Jafa ✍ ℳaahali: Dar es salaam🇹🇿 ₩h...
No comments:
Post a Comment